Jumatatu 20 Oktoba 2025 - 07:54
Ayatullah Khaalisiy atoa onyo kali kuhusiana na muelekeo wa baadhi ya harakati za Iraq kuuelekea “mradi wa Marekani”

Hawza/ Ayatullah Sheikh Jawad Khaalisiy amezionya baadhi ya harakati za kisiasa za Iraq kujiunga na “mradi wa Marekani”, akisisitiza kuwa taasisi za kiusalama zinatawaliwa na watu wanaotumikia maslahi ya Marekani.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sheikh Jawad Khaalisiy, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Iraq, katika mahojiano na kituo cha televisheni Al-Mayadeen Plus, alisema kuwa Wamarekani wamewaalika Wairaq na wengine kushiriki katika mradi wanaouita “mradi wa ukombozi”.
Akaeleza kuwa: “Baadhi ya makundi ambayo hapo awali yalikuwa yakipinga mradi wa Marekani, hivi sasa yameanza kuelemea upande wake na kujishughulisha na kuusifu na kuutetea.”

Mwanazuoni huyu mashuhuri wa Iraq akizungumzia kushindwa kwa baadhi ya harakati za kisiasa zikiwemo zile za Kiislamu, alibainisha kuwa: “Kushindwa huko kulitokana na ukweli kwamba harakati hizo zilianza misingi yake kwa kutegemea miradi ya kigeni.”

Akaongeza tena: “Kuna uamuzi wa kisiasa wa kulazimishwa unaozuia utatuzi wa matatizo ya maisha ya wananchi na ujenzi mpya wa miundombinu ya Iraq. Lengo kuu ni kuirudisha Iraq kwenye siku zile za machafuko makubwa, ilhali wananchi wamegharamikia mno ili kupata usalama.”

Ayatullah Khaalisiy alisema pia: “Taasisi za usalama zinatawaliwa na watu wanaohusishwa na Marekani, na jeshi limekuwa lisilo na uwezo wa kuchukua hatua madhubuti.”

Aidha, alikosoa baadhi ya watu wanaodai kuwa wawakilishi wa Marja‘iyya (uongozi wa kidini) kwa kutumia vibaya hali ya sasa na kudhoofisha umoja wa kitaifa unaolenga uhuru wa Iraq.

Mwanazuoni huyu wa Iraq alisisitiza zaidi akisema: “Mchukuaji wa maamuzi muhimu na mwenye ushawishi mkubwa nchini Iraq si Iran, bali ni Marekani, na ndani ya nchi kuna ushawishi wa siri na hatari wa Kizayuni.”

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Ayatullah Khaalisiy alizungumzia msimamo wa Iraq katika masuala ya eneo na akasema: “Ingawa Iraq imechukua msimamo thabiti na wenye nguvu kuhusiana na matukio ya Ghaza, lakini kutokana na uzito wake wa kisiasa na kijiografia, nchi hii ina uwezo wa kuchukua nafasi kubwa na yenye athari zaidi.”

Mwisho wa mazungumzo yake, alisisitizia kuwa: “Mikono ya muqawama huko Ghaza imepata ushindi, Netanyahu ameshindwa, na kujitolea kwa Hizbullah na Iran kunadhihirisha kuwa vita vya kieneo bado vinaendelea.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha